Jinsi ya kuanzisha biashara ya mgahawa
Ujasiriamali
by Ali Mwambola
Baadhi ya wafanyabiashara wanafikiri biashara ya mgahawa ni rahisi kuanzisha na kupata mafanikio. Lakini hali halisi ni tofauti kabisa, kwani usipokuwa makini, unaweza kujikuta kwenye matatizo makubwa ya kibiashara. Kama wewe unataka kuanzisha biashara ya mgahawa, ni muhimu uwe makini kwa sababu hii ni biashara inayotoa huduma ya chakula na vinywaji kwa wateja. Wateja wanataka chakula kilichopikwa vizuri na mazingira ya mgahawa yawe ya kuvutia. Vile vile wateja wanataka wafanyakazi wa mgahawa wawe nadhifu, wachangamfu na wanaojali wateja. Kama umekuwa na ndoto ya kuanzisha mgahawa jambo la kwanza linalokuja kwenye mawazo yako ni suala la dhana (concept) ya mgahawa.
Uchaguzi wa dhana ya mgahawa ni hatua muhimu katika uanzishaji wa biashara ya mgahawa. Dhana ya mgahawa inatakiwa kujumuisha aina ya mgahawa unaotaka kuanzisha, vyakula mbali mbali vitakavyokuwa vinapikwa kwenye mgahawa na aina ya huduma itakayotolewa kwa wateja wa mgahawa. Muonekano wa ndani wa mgahawa ni lazima ulingane na dhana inayotumika kuanzisha mgahawa mpya
Mifano ya dhana mbali mbali za migahawa ni kama ifuatavyo:
* Mgahawa kwa ajili ya kuuza vyakula kwa wateja wasiokaa mgahawani (take away customers)
* Mgahawa kwa ajili ya kuuza vyakula vya chips, kuku na mayai
* Mgahawa kwa ajili wateja wanaokaa mgahawani na kuagiza chakula
Ni muhimu pia uchague chapa ya mgahawa ambayo itakupa mafanikio kibiashara. Chapa ya mgahawa itakuwa ni kiungo cha mawasiliano kuhusu dhamira na utambulisho wa mgahawa. Jina la mgahawa, nembo ya mgahawa, menu ya chakula na, bidhaa na huduma vinatakiwa kwa pamoja kuonyesha chapa ya mgahawa. Matangazo utakayokuwa unatoa kwa ajili ya mgahawa yanatakiwa yazingatie utambulisho na chapa ya mgahawa ambavyo vitasaidia kuonyesha jinsi mgahawa uavyotoa huduma. Kama umekwisha chagua eneo la kufanya biashara ya mgahawa inabidi uhakikishe kuwa aina ya wateja utakao hudumia ndio watatumika kutengeneza dhana (concept) ya mgahawa